Mkuu wa Operesheni wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon
Siro (54) (pichani), amedai mahakamani kuwa alitoa zuio la kuandamana
kwenda Ikulu kwa wanachama wa Baraza la Wanawake (Bawacha) kwa sababu
maandamano hayo yangesababisha uvunjifu wa amani.
Alitoa madai hayo wakati akitoa ushahidi mbele ya Hakimu Mkazi
Janeth Kaluyenda, katika kesi inayomkabili Mwenyekiti wa Bawacha, Halima
Mdee na wenzake, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es
Salaam jana.
Alidai baada ya kupitia vigezo vya kiusalama, walibaini kuwa njia
waliyotaka kuitumia kufanya maandamano hayo inatumiwa na watu wengi,
hivyo alishughulikia mara moja kuzuia maandamano hayo.
Akiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Tumaini Kweka, shahidi
huyo alidai kuwa Oktoba 2, mwaka huu alipokea barua iliyopitia kwa
Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, kutoka Bawacha
wakiomba kufanya maandamano ya amani kwenda Ikulu.
“Katika barua hiyo, Bawacha waliomba kufanya maandamano kwenda
Ikulu kwa Rais Jakaya Kikwete kumtaka asipokee katiba
inayopendekezwa…maandamano hayo yalipangwa kufanyika Oktoba 4, mwaka
2014 saa 3:00 asubuhi,” alidai Siro na kuiomba mahakama ipokee nakala ya
barua hiyo kama kielelezo, lakini yakatokea mabishano ya kisheria.
Kesi iliahirishwa hadi Machi 3, mwaka huu, ushahidi utakapoendelea kusikilizwa.
0 comments:
Post a Comment