Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo, amesema watu wote waliohusika
‘kuiba’ mtoto mwenye ulemavu wa ngozi (albino), Pendo Emmanuel (4),
katika Kijiji cha Ndami, Wilaya ya Kwimba, mkoani humo wamekamatwa.
Akizungumza wakati akiwaapisha wakuu wapya wa wilaya wa mkoa huo
jana, Manju Msambya (Misungwi), Zainab Rajab (Sengerema) na Pili Moshi
(Kwimba), Mulongo alisema watu wote waliohusika wamekamatwa na hivi
sasa bado hawafahamu kama mtoto huyo yupo hai ama mfu.
“Wezi wale baada ya kumuiba mtoto Pendo walimleta katika hoteli
moja hapa jijini Mwanza, kisha kuwakabidhi watu walioonekana wanunuzi,
lakini wote hao wamekamatwa akiwamo mmiliki wa hoteli hiyo,” alisema
Mulongo.
Alisema serikali ipo kazini wakati wote, ndiyo maana inafanya kazi
usiku na mchana kuwasaka watu wote waovu mkoani Mwanza ambao hawawezi
kusalimika kwa kile watakachokifanya.
Hata hivyo, alisema watu hao waliofanya uhalifu huo akiwamo baba wa
mtoto huyo, Emmanuel Shilinde, wanashikiliwa na polisi huku mtu wa
mwisho aliyetoweka na mtoto huyo toka hotelini hapo akiendelea
kutafutwa.
Katibu wa Chama cha Maalbino Mkoa wa Mwanza, Mashaka Tuju,
aliishutumu serikali kwa kushindwa kuchukua hatua stahili tangu mauaji
ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) yalipoanza miaka tisa iliyopita.
Katika kipindi cha miezi miwili, watoto Pendo Emmanuel wa Kwimba na
Yohana Bahati (mwaka mmoja) wa Kijiji cha Ilelema, wilayani Chato,
walitekwa na watu wasiojulikana.