Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA) iliundwa kwa tamko la Serikali la mwaka 1973, lengo kubwa likiwa kupanga mji, kuishauri na kuisaidia Serikali kuhamia Dodoma.
Wazo la kuhamia Dodoma lililotamkwa miaka 42 iliyopita, enzi za utawala wa Rais wa Kwanza wa Tanzania, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, limegeuka kama wimbo machoni pa watu na linatekelezwa kwa kusuasua. Hata hivyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Uratibu na Bunge), Jenista Mhagama anasema azma ya Serikali kuhamia Dodoma bado iko palepale na mchakato unaendelea.
“Serikali ipo katika mchakato wa kuandaa sheria ya kuhamia Dodoma,” anasema Mhagama.
Lakini CDA iliyopewa majukumu ya kushauri katika mradi huo inaeleza kuwa kasi ndogo ya uhamiaji wa Dodoma inasababishwa na mtazamo wa wahusika.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa CDA, Paskasi Muragili anasema awali jukumu la kuendeleza mji wa Dodoma liliachwa kwa Serikali Kuu pekee, huku sekta binafsi na taasisi nyingine zikiwa kando.
“Serikali imebadilisha mtazamo wake, sasa mji wa Dodoma utajengwa na Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi,” anasema Muragili.
“Sekta binafsi inaweza kujenga sehemu ya huduma muhimu. Kwa hiyo Serikali haijahamia kwa sababu hakuna mazingira yanayoiwezesha kuwa hapa Dodoma,” anasema Muragili.
Viongozi kuchochea migogoro
Akizungumzia suala la baadhi ya viongozi kuchochea migogoro akiwamo yeye, Muragili anasema miradi mingi ya CDA imekuwa ikikwama kutekelezwa kwa sababu ya matakwa ya kisiasa.
“Nimekuwa nikisikia kuwa nina mgogoro na CDA, lakini binafsi nikiwa nao, sioni mgogoro huo,” anasema.
Anasema tangu aliposhika nafasi hiyo, amehudhuria vikao vya madiwani mara mbili kwa ajili ya utendaji wa mji na walifikia makubaliano.
“Pia tumekuwa na semina ileyolenga kuzungumzia namna tutakavyokwenda katika utendaji wa pamoja, ambapo tulifikia maazimio fulani,” anasema Muragili na kuongeza:
 Lakini zipo kauli za wanasiasa zinazokwenda tofauti na tunayotenda. Hili ndilo linanifanya nishindwe kukiri kuwa kuna mgogoro kati yetu na madiwani,” anasema.
Anasisitiza kuwa suala hilo ni la kisiasa na kwamba utendaji wao wa kazi umekuwa ukiungwa mkono na manispaa.
Hata hivyo, anasema changamoto kubwa nyingine ni wananchi kutofuata taratibu za uendelezaji wa Mji wa Dodoma.
Anasema kwa sasa CDA haitabomoa nyumba zilizojengwa kinyume cha taratibu, bali cha muhimu ramani ya Mipango Miji (Master Plan) ionyeshe kuwa eneo husika limetengwa kwa makazi.
Anasema kitakachofanyika katika maeneo hayo ni kuboresha tu na wala siyo kubomoa.
“Kama ni eneo kwa ajili ya shule, barabara au miundombinu mingine tutabomoa ili kuupanga mji,” anasema.
Akizungumzia tatizo hilo, Waziri Mhagama anawataka viongozi kutoa kauli za busara, badala ya zile zinazoweza kuibua uchochezi kwenye jamii.
Anasema ushirikiano wa CDA na wananchi umeimarika, hivyo kuondoa vurugu zilizokuwa zikijitokeza wakati wa upimaji wa viwanja.
Udalali wa viwanja
Akizungumzia kujitokeza kwa udalali wa viwanja, Muragili anasema: “Ni kweli kumekuwa na tatizo la udalali wa viwanja. Nilipoingia katika nafasi hii mwaka 2012, tulifanya uchunguzi na kugundua kuwa sababu ya kwanza ni ukosefu wa viwanja vilivyopimwa.
Hatua yetu ya kwanza ilikuwa kuhakikisha tunapima viwanja vingi na tumeweza kupima viwanja 10,000 kati ya hivyo 5,000 vimekwenda katika mikono ya wananchi.”
Anabainisha kuwa kwa sasa mji wa Dodoma una viwanja 5,000 vinavyoweza kutolewa hivi karibuni.

Advertisement

0 comments:

 
Top