Licha  ya kuwa na matokeo mabaya na kufungwa mabao 8-0 dhidi ya Yanga Jumatano, uongozi wa Coastal Union umesema hautamfungashia virago kocha mkuu wao wa muda, Jamhuri Kihwelo 'Julio', imeelezwa.
 
Tangu kutua kwa kocha mkuu huyo wa Mwadui FC jijini Tanga, Wagosi wa Kaya, wameshinda mechi mbili dhidi ya Mgambo na JKT Ruvu huku timu ikipoteza mechi tatu dhidi ya Azam FC, Prisons na Yanga pamoja na sare mbili dhidi ya Kagera Sugar na Ruvu Shooting.
 
Hata hivyo, uongozi wa Coastal Union kupitia kwa msemaji wake, Oscar Assenga, ulikanusha taarifa zilizoenea kwamba Julio aliambiwa afungashe virago baada ya kipigo cha fedheha cha mabao 8-0 dhidi ya Yanga.
 
"Julio ataendelea kuwa kocha wetu hadi mwisho wa msimu huu. Baada ya hapo timu itakuwa chini ya Joseph Lazaro (kocha msaidizi wa Coastal aliyeipandisha Africans Sports ligi kuu msimu ujao)," alisema.
 
Mara tu baada ya kumalizika kwa mechi yao dhidi ya Yanga kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Jumatano, Julio 
alizungumza waandishi wa habari na kuweka wazi kwamba kamwe hatajiuzulu kutokana na kipigo hicho kikubwa katika maisha yake ya ukocha.
 
"Sifikirii kujiuzulu, nijiuzulu kwa sababu gani? Kama nikujiuzulu, angeanza kocha wa Brazil (waliofungwa 7-1 dhidi ya Ujerumani kwenye Kombe la Dunia) na vigogo wa Ikulu waliochota fedha za walipa kodi na wanasiasa wanaoiba fedha za vyama na serikali," alisema Julio.
 
Kikiwa chini ya Julio, kikosi cha  mabingwa wa 1988 wa Tanzania Bara, Coastal Union, kilisahihisha makosa ya kufungwa 8-0 dhidi ya Yanga na kuilaza JKT Ruvu kwa mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Azam jijini Dar es Salaam juzi.
 
Mshambuliaji Mkenya Rama Salim alifunga kwa penalti dakika ya 10 kabla ya mshambuliaji mwenzake Ike Bright kufunga la pili kwa shuti la mguu wa kulia na kuiondoa timu yao katika hatari ya kuporomoka daraja ikipanda kwa nafasi tano kutoka nafasi ya 11 hadi ya sita (kabla ya mechi za jana).

Advertisement

0 comments:

 
Top