Rais Jakaya Kikwete, amewataka viongozi wa dini kutoruhusu siasa
kufanyika katika nyumba za ibada, kwani kufanya hivyo kutalifanya taifa
liingie kwenye machafuko.
Rais Kikwete alitoa rai hiyo jana wakati wa ibada ya kuwekwa wakfu
na kusimikwa Askofu mpya wa Kanisa Katoliki Jimbo la Shinyanga,
Liberatus Sangu, iliyofanyika Kanisa Kuu la Mama Mwenye Huruma Ngokolo
mjini Shinyanga na kuongozwa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es
Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo.
Alisema katika kipindi cha kuelekea Uchaguzi Mkuu, baadhi ya
wanasiasa na washirika wao wamekuwa wakizunguka kwenye nyumba za ibada
na kuzungumza mambo ya siasa, hali inayosababisha kuwagawa waumini
makundi ambayo yanaweza kusababisha machafuko kutokana na tofauti za
itikadi ya vyama vyao.
“Viongozi wa dini kuweni makini, msiwape nafasi watu hawa msiruhusu wanasiasa kuchukua nafasi makanisani ili tujenge taifa,
hakikisheni makanisa yanabaki kuwa sehemu ya ibada na wala si majukwaa ya siasa,” alisema Rais Kikwete.
Alisema viongozi wa dini wanatakiwa kutoruhusu siasa kuingia kwenye
dini na dini kuingizwa kwenye siasa, iwapo itafanikiwa kufanyika kwa
hayo wataokoa mambo mengi na wanasiasa kuacha kukimbilia katika nyumba
za ibada. Alitahadharisha kuwa, kuwaruhusu wanasiasa kuingia nyumba za
ibada kutasababisha hatari ya uvurugaji wa amani na utulivu wa taifa.
“Kama tutafika huko kitachotokea ni wakati wa kushindwa kwa chama
cha siasa sawa na kushindwa kwa dini ambayo ilikuwa inaunga mkono chama
hicho, hivyo kusababisha mgogoro kutokea hali ambayo itasababisha
machafuko katika taifa letu,” alisema.
Hata hivyo, alisema kiongozi wa siasa akienda kanisani inabidi
akaribishwe, lakini pale atakapoanza masuala ya siasa
inawalazimu kumwambia hapo siyo mahali pake na haparuhusu kuwapo jukwaa
la kisiasa.
MAUAJI YA ALBINO
Katika hatua nyingine, Rais Kikwete aliwataka viongozi wa dini
kuwaelimisha wananchi kutoendekeza imani za kishirikina zinazosababisha
mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) na vikongwe, kwani
vitendo hivyo vinachafua sifa ya nchi kimataifa.
Alisema serikali itaendelea kushirikiana na taasisi za dini ili
kuhakikisha Tanzania inaendelea kuwa mahali pa amani, upendo, mshikamano
na utulivu.
RAIS WA TEC
Awali, Rais wa Baraza la Maaskofu Kanisa Katoliki Tanzania (TEC),
Tarcisius Ngalalekumtwa, alimpongeza Askofu Liberatus Sangu kwa
kusimikwa kuwa Askofu wa jimbo hilo baada ya miaka mitatu tangu
alipofariki Askofu Aloysius Balina mwaka 2012.
ASKOFU SANGU
Akizungumza baada ya kuwekwa wakfu na kusimikwa rasmi, Askofu Sangu
aliahidi kushirikiana na serikali katika kuongoza waumini katika
kutenda yaliyo mema mbele za Bwana ili kudumisha amani ya taifa.
0 comments:
Post a Comment